Maria Zakharova alisema hayo jana katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram, ambapo amezitolewa mwito taasisi za kimataifa kuichukulia kwa uzito taarifa iliyotolewa mwezi uliopita na Idara ya Usawa wa Kijinsia ya Sweden.
Taasisi hiyo ya serikali ya Sweden ilionya katika ripoti yake kuwa, wakimbizi wa Ukraine walioko katika nchi hiyo ya Ulaya wanaandamwa na magendo ya binadamu, kutumikishwa na kutumbukia katika ukahaba.
Ripoti ya Idara ya Usawa wa Kijinsia ya Sweden ilieleza kuwa, kumekuwa na ongezeko la idadi ya makahaba kutoka Ukraine nchini humo, tangu mgogoro baina ya Kiev na Moscow uanze mwishoni mwa Februari mwaka huu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amefafanua kuwa, licha ya ripoti hiyo kuakisiwa pakubwa na vyombo vya habari vya Sweden, lakini hakuna hatua yoyote iliiyochukuliwa na Ukraine au jamii ya kimataifa.
Maria Zakharova amesisitiza kuwa, "Tishio halisi kwa wanawake wa Ukraine halitokani na Russia, lakini linawasubiri katika nchi za Ulaya."
Ameongeza kwa kusema, UN na taasisi za haki za binadamu zimenyamazia kimya unyanyasaji wa kijinsia unaowasakama wanawake wakimbizi wa Ukraine katika nchi za Ulaya, kwa kuwa ama hazishughulishwi na matatizo halisi ya kibinadamu, au kwa kuwa hivi sasa zinatekeleza amri nyingine ya kisiasa ya mabwana zao.
342/